Usambazaji wa Vifaa vya CEmONC, Mikoa ya Dodoma na Singida
Bohari ya Dawa (MSD) kupitia Kanda yake ya Dodoma inayohudumia Mikoa ya Singida na Dodoma, imeendelea na ugawaji wa vifaa vya Huduma Kabambe za Uzazi na Uzazi wa Watu Wapya (CEmONC).
Akizungumzia ugawaji huo Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma Bw.John Sipendi amesema kuwa ugawaji wa vifaa hivyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vinavyohudumiwa na Kanda yake ya Dodoma ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuboresha huduma za dharura za mama na mtoto.
Alibainisha kuwa Kanda yake kwa sasa inatekeleza ugawaji kwa takriban vituo 26 vya kutolea huduma za afya vilivyoainishwa kwa ajili ya kusambaza vifaa hivyo katika Mikoa ya Singida na Dodoma.
“Ikumbukwe kuwa Rais amekuwa akiweka wazi kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali katika awamu hii ya 6 ni kuhakikisha inaboresha huduma hasa zile zitakazopunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua”. Alisema Sipendi
Meneja Sipendi amesisitiza kuwa ataendelea kuhakikisha vifaa vyote vinavyoletwa kutoka makao makuu vinasambazwa kwa wakati na haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopangwa.
Hata hivyo, pamoja na usambazaji wa vifaa vya CEmONC, Kanda ya Dodoma pia imeendelea kusambaza bidhaa nyingine za afya kwa takriban vituo 685 vya kutolea huduma za afya katika Mikoa ya Singida na Dodoma.