Ununuzi
Bohari ya Dawa (MSD) ni taasisi iliyokasimishwa jukumu la ununuzi wa bidhaa za afya kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wake. Bidhaa zinazonunuliwa na MSD hutumika kwa ngazi zote za vituo vya kutolea huduma ya afya kuanzia zahanati hadi hospitali za Taifa.
Ununuzi wa bidhaa za afya huzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2024 na zabuni zote hutangazwa kupitia Mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma unaojulikana kama NeST (National e-Procurement System), unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
MSD ni mnunuzi mkubwa wa bidhaa za afya nchini, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa za afya hununuliwa kutoka nchi mbalimbali duniani. Katika kuongeza ufanisi kwa kupunguza muda wa uagizaji, ubora wa bidhaa na gharama, Bohari ya Dawa imekuwa ikinunua sehemu kubwa ya bidhaa za afya kutoka moja kwa moja wazalishaji wa ndani na wale wa nje ya nchi, na kuwa kichochezi cha uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya nchini.
Bidhaa za afya zinazonunuliwa na Bohari ya Dawa hupitia mchakato mzima wa kuhakikisha zinakuwa na ubora kwa kuhitaji uthibitisho wa usajili au uthibati kutoka mamlaka za simamizi zikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC).
Kila bidhaa hupitia mchakato makini wa tathmini ya ubora, usalama, ufanisi, na uthabiti, ili kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi viwango na muda wa matumizi uliowekwa.