Kanda ya Mbeya
Kanda ya MSD Mbeya ilianzishwa mwaka 1998 kama kituo cha mauzo kikiwekwa kimkakati kuhudumia mikoa ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Mwaka 2000, kituo hiki kilipandishwa hadhi na kuwa Ofisi Kamili ya Kanda, hatua iliyoipa mamlaka na uhuru zaidi wa kusimamia na kuendesha shughuli zake.
Mawanda ya Utoaji Huduma
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kanda ya MSD Mbeya inahudumia jumla ya watu 5,338,120. Idadi hii inajumuisha;
Mkoa wa Mbeya: watu 2,343,754,
Mkoa wa Rukwa: watu 1,540,519,
Mkoa wa Songwe: watu 1,344,687,
Mkoa wa Njombe (Wilaya ya Makete) :watu 109,160
Kanda ya MSD Mbeya inahudumia jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 979, ikijumuisha vituo kuanzia ngazi ya msingi, ngazi ya kati, hadi ngazi ya taifa.
1. Vituo ngazi ya kati na taifa – Hospitali ya Rufaa ya Kanda 1, na hospitali za Rufaa za Mikoa 5.
2. Vituo ngazi ya msingi – Hospitali 16 za wilaya zilizo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – (TAMISEMI), hospitali teule 9 za Wilaya, vituo vya afya 88, na zahanati 806,
3. Vituo vya Tasisi za kidini na taasisi nyingine za umma - Taasisi za kidini 17 na taasisi nyingine za umma 39.
Uwezo wa Uhifadhi na Uendeshaji
Ili kuhudumia vituo vya afya ipasavyo na kwa ufanisi, kanda hii ina ghala lenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 5,340 na magari 16 ya usambazaji yenye ukubwa tofauti kulingana na mahitaji. Rasilimali hizi kwa pamoja huiwezesha Kanda kutunza, na kusambaza dawa na vifaa tiba kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na usalama.
Mafanikio ya kanda ya MSD Mbeya yanatokana na uwapo wa timu ya wataalamu 36 ikihusisha wabobezi wa masuala ya ugavi ,wafamasia, wahasibu, wawakilishi wa mauzo, maofisa huduma kwa wateja, mafundi sanifu vifaa tiba na madereva. Mchango wao wa kitaalamu unahakikisha kuwa kanda hii inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa usambazaji katika maeneo yake.
Utoaji wa Huduma Bora
Kwa kuzingatia eneo lake la kimkakati, miundombinu ya kisasa, na nguvu kazi yenye ujuzi, Kanda ya MSD Mbeya inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya mikoa ya Kanda ya ziwa nchini Tanzania.
Kanda hii pia, inaendelea kujidhatiti kutekeleza dira kuu ya MSD ya kuwa "Kituo Bora cha Umahiri katika Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya Barani Afrika".