Ruka kwenda maudhui makuu

Uzalishaji

Mnamo mwaka 2021, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipanua majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD) kupitia Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Written Laws – Miscellaneous Amendments) (Sheria Na. 4 ya mwaka 2021), na kuiwezesha taasisi hiyo kujihusisha rasmi na uzalishaji wa bidhaa za afya. Mageuzi haya muhimu yalilenga kuimarisha muundo wa mnyororo wa upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, sambamba na utekelezaji wa ajenda ya serikali ya viwanda, kwa kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuhakikisha upatikanaji mpana wa bidhaa bora, salama na zenye gharama nafuu zinazozalishwa nchini.

Ili kutekeleza dira hii, MSD ilianzisha Kampuni ya MSD Medipharm Manufacturing Company Limited mwaka 2023, ikiwa ni kampuni tanzu inayomilikiwa kwa asilimia 100 na MSD, yenye jukumu la uzalishaji wa bidhaa za afya. Mkakati huu unalenga kuiwezesha MSD kuendelea kuzingatia majukumu yake ya msingi ya ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya, huku ukihakikisha ufanisi, uwajibikaji na uhamasishaji wa rasilimali katika mnyororo mzima wa thamani.

Kwa sasa, MSD Medipharm Manufacturing Company Limited inaendesha viwanda vya uzalishaji wa barakoa (masks) jijini Dar es Salaam na glavu za tiba mkoani Njombe. Aidha, kampuni inasimamia kongani ya viwanda vya Dawa (Pharmaceutical Industrial Park) iliyopo Zegereni – Kibaha, ambayo imebuniwa kuvutia wawekezaji, kukuza ubia wa kimkakati na kuharakisha uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi. Tayari MSD imeagazia fursa za uwekezaji kwenye bidhaa za pamba, condom, na nyinginezo ambapo tayari imeanza kushirikiana na wawekezaji wengine kuanzisha uzalishaji. Kongani hii inafanya kazi kama kichocheo cha uhamishaji wa teknolojia, ukuzaji wa ujuzi na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa viwanda vya ndani.

Kwa kuzingatia kaulimbiu ya MSD isemayo Tumedhamiria Kuokoa Maisha”, dhamira ya Medipharm ni kuzalisha na kusambaza bidhaa za afya zenye ubora wa juu, salama na gharama nafuu, kwa lengo la kuunga mkono na kuimarisha mfumo wa huduma za afya nchini. Kupitia ushirikiano wa kimkakati na sekta binafsi, kutoka ndani na nje ya nchi, Medipharm inaendelea kuhimiza ubunifu, kupanua uwezo wa uzalishaji na kuhakikisha upatikanaji wa uhakika, endelevu na shindani wa bidhaa muhimu za afya.

Kwa kuhamasisha uzalishaji wa ndani, Medipharm haichangii tu kujenga uwezo wa taifa kujitegemea katika sekta ya afya, bali pia inafungua fursa za ukuaji wa masoko ya kikanda, na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu na lango la uzalishaji wa bidhaa za afya, Mashariki na Kusini mwa Afrika.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.