Kanda ya Dar es Salaam
Kanda ya Dar es Salaam ya Bohari ya Dawa ni mojawapo ya Kanda 10 za MSD, iliyoanzishwa kimkakati mwaka 2009, kama kitovu muhimu cha mtandao wa kitaifa wa ugavi wa bidhaa za afya mashariki mwa Tanzania.
Kanda ya Dar es Salaam inahudumia mikoa mitatu ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam yenyewe, Pwani na Morogoro. Vilevile, kanda hii imepanua wigo wa huduma zake hadi Zanzibar, kutokana na ukaribu wake kijiografia ili kusaidia upatikanaji wa bidhaa za afya visiwani humo.
Mawanda ya Utoaji Huduma
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, MSD Kanda ya Dar es Salaam inahudumia jumla ya watu 12,495,552. Idadi hii inajumuisha watu kutoka mikoa hii kama ifuatazo:
Mkoa wa Dar es Salaam – watu 5,383,728.
Mkoa wa Pwani – watu 2,024,947.
Mkoa wa Morogoro – watu 3,197,104.
Zanzibar – takribani watu 1,889,773.
Kanda ya MSD Dar es Salaam inahudumia jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 1,116, ikijumuisha vituo kuanzia ngazi ya msingi, ngazi ya kati, hadi ngazi ya taifa.(primary,secondary and tertiary-level)
1. Vituo ngazi ya kati na taifa – Hospitali ya taifa 1, Maabara ya Taifa 1, hospitali bobezi 5, hospitali za Rufaa za Mikoa 06.
2. Vituo ngazi ya msingi – Hospitali za wilaya 14 zilizo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – (TAMISEMI), vituo vya afya 98, na zahanati 824.
3. Vituo vya Tasisi za kidini na taasisi nyingine za umma - Taasisi za kidini 26 na nyingine za umma 142, pamoja na Zanzibar.
Uwezo wa Uhifadhi na Uendeshaji
Ili kuhudumia vituo vya afya ipasavyo na kwa ufanisi, kanda hii ina ghala lenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 12,000 na magari 20 ya usambazaji yenye ukubwa tofauti kulingana na mahitaji. Rasilimali hizi kwa pamoja huiwezesha Kanda kutunza, na kusambaza dawa na vifaa tiba kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na usalama.
Mafanikio ya kanda ya MSD Dar es Salaam yanatokana na uwapo wa timu ya wataalamu 29 ikihusisha wabobezi wa masuala ya ugavi ,wafamasia, wahasibu, wawakilishi wa mauzo, maofisa huduma kwa wateja, mafundi sanifu vifaa tiba na madereva. Mchango wao wa kitaalamu unahakikisha kuwa kanda hii inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa usambazaji katika maeneo yake.
Utoaji wa Huduma Bora
Kwa kuzingatia eneo lake la kimkakati, miundombinu ya kisasa, na nguvu kazi yenye ujuzi, Kanda ya MSD Dar es Salaam inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya mikoa ya mashariki mwa Tanzania.
Kanda hii pia, inaendelea kujidhatiti kutekeleza dira kuu ya MSD ya kuwa "Kituo Bora cha Umahiri katika Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya Barani Afrika".