Kanda ya Tabora
Kanda ya Tabora ya Bohari ya Dawa (MSD) ilianzishwa mwaka 1997. Kanda hii ya MSD ni miongoni mwa kanda za muda mrefu zaidi, ikiwa ni kitovu muhimu cha mtandao wa kitaifa wa ugavi wa bidhaa za afya magharibi mwa Tanzania. Ofisi za kanda ya Tabora ziko katika Manispaa ya Tabora, na kanda hii inahudumia jumla ya mikoa mitatu, ambayo ni Tabora, Katavi, na Kigoma.
Mawanda ya Utoaji Huduma
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania ya mwaka 2022, Kanda ya MSD Tabora inahudumia takribani watu 7,015,604. Idadi hii inahusisha mikoa ya Tabora, Katavi, na Kigoma:
Mkoa wa Tabora watu 3,391,679,
Mkoa wa Katavi watu 1,152,958 na
Mkoa wa Kigoma watu 2,470,967).
Kanda ya MSD Tabora inahudumia jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 842, ikijumuisha vituo kuanzia ngazi ya msingi, ngazi ya kati, hadi ngazi ya taifa.
1. Vituo ngazi ya kati na taifa – Hospitali za Rufaa za Mikoa 3.
2. Vituo ngazi ya msingi – Hospitali za wilaya 21, zilizo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – (TAMISEMI), hospitali teule ya Wilaya 1, vituo vya afya 95, na zahanati 705,
3. Vituo vya Tasisi za kidini na taasisi nyingine za umma - Taasisi za dini 16 na taasisi nyingine za umma 6.
Uwezo wa Uhifadhi na Uendeshaji
Ili kuhudumia vituo vya afya ipasavyo na kwa ufanisi, kanda hii ina ghala lenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 2,700 na magari 17 ya usambazaji yenye ukubwa tofauti kulingana na mahitaji. Rasilimali hizi kwa pamoja huiwezesha Kanda kutunza, na kusambaza dawa na vifaa tiba kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na usalama.
Mafanikio ya kanda ya MSD Tabora yanatokana na uwapo wa timu ya wataalamu 41 ikihusisha wabobezi wa masuala ya ugavi ,wafamasia, wahasibu, wawakilishi wa mauzo, maofisa huduma kwa wateja, mafundi sanifu vifaa tiba na madereva. Mchango wao wa kitaalamu unahakikisha kuwa kanda hii inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa usambazaji katika maeneo yake.
Utoaji wa Huduma Bora
Kwa kuzingatia eneo lake la kimkakati, miundombinu ya kisasa, na nguvu kazi yenye ujuzi, Kanda ya MSD Tabora inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya mikoa ya Kanda ya ziwa nchini Tanzania.
Kanda hii pia, inaendelea kujidhatiti kutekeleza dira kuu ya MSD ya kuwa "Kituo Bora cha Umahiri katika Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya Barani Afrika".