Ruka kwenda maudhui makuu

Usambazaji

Bohari ya Dawa (MSD) ina mtandao imara na wenye ufanisi wa kitaifa wa mnyororo wa ugavi unaohakikisha bidhaa za afya zinafika kwa wakati kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Mnyororo wa ugavi huanzia katika Maghala Makuu ya Bohari ya Dawa yaliyopo Dar es Salaam na Dodoma na kuendelea kupitia Maghala ya Kanda zake, yaliyopo Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Iringa, Dodoma, Tabora, Mwanza, Kilimanjaro, Tanga, na Kagera yaliyowekwa kimkakati nchi nzima. Usambazaji wa bidhaa za afya hufanywa kwa kutumia barabara, reli, maji pamoja na anga, hivyo kuhakikisha bidhaa zinafika maeneo yote nchini kwa kutumia vyombo vya usafiri vya sekta ya umma pamoja na binafsi.

MSD inamiliki magari zaidi ya 200 ya usafirishaji ya aina mbalimbali yakiwemo Land Cruiser, MAN truck, Scania, na Iveco, ambayo kwa pamoja yanahudumia takribani vituo vya kutolea huduma za afya 9,000 nchi nzima, ikijumuisha hospitali za Taifa, hospitali maalum, hospitali za Kanda, hospitali za Rufaa za Mikoa, hospitali za wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati kwa utaratibu maalum wa usambazaji wa kila baada ya miezi miwili. Mfumo huu wa usambazaji wa moja kwa moja hadi mlangoni kwa vituo (direct delivery) umeongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa utoaji huduma, na kuboresha kiwango cha upatikanaji wa mahitaji ya bidhaa za afya kwa wateja.

Kila mzigo wa bidhaa unaosafirishwa na kukabidhiwa huthibitishwa kupitia Fomu ya Uthibitisho wa Uwasilishaji, ambayo pia huwa kwenye mfumo wa kidijitali na huonesha jina la mpokeaji wa bidhaa husika, anwani yake, maelezo ya bidhaa, idadi na tarehe ya uwasilishaji, ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika mnyororo mzima wa ugavi.

Bidhaa zinazowasilishwa hukabidhiwa rasmi kwa kamati za afya za vituo husika vya kutolea huduma za afya, hivyo kuimarisha dhamira ya MSD ya uaminifu, uadilifu na ubora katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.