Kanda ya Kilimanjaro
Kanda ya Kilimanjaro ya Bohari ya Dawa (MSD) ilianzishwa kimkakati mwaka 1998, ikiwa na jukumu muhimu la ugavi wa uhakika wa dawa na vifaa tiba bora katika vituo vya huduma za afya katika mikoa ya upande wa kaskazini mwa Tanzania.
Kanda hii ya MSD Kilimanjaro inahudumia jumla ya mikoa ya 3, ambayo ni Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Mawanda ya Utoaji Huduma
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania ya mwaka 2022, MSD kanda ya Kilimanjaro inahudumia takribani watu 5,758,386. Idadi hii ya watu inajumuisha;
Kilimanjaro-watu 1,861,934,
Arusha-watu 1,540,519 na
Manyara-watu 1,892,502
Kwa ujumla Kanda ya MSD Kilimanjaro inahudumia jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 856, ikijumuisha vituo kuanzia ngazi ya msingi, ngazi ya kati, hadi ngazi ya taifa.
1. Vituo ngazi ya kati na taifa – Hospitali bobezi 1, Hospita ya Rufaa ya Kanda 1, na hospitali za Rufaa za Mikoa 3.
2. Vituo ngazi ya msingi – Hospitali za wilaya 18, zilizo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – (TAMISEMI), hospitali teule ya Wilaya 1, vituo vya afya 95, na zahanati 590.
3. Vituo vya Tasisi za kidini na taasisi nyingine za umma - Taasisi za dini 73 na taasisi nyingine za umma.
Uwezo wa Uhifadhi na Uendeshaji
Ili kuhudumia vituo vya afya ipasavyo na kwa ufanisi, kanda hii ina ghala lenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 1,786 na magari 14 ya usambazaji yenye ukubwa tofauti kulingana na mahitaji. Rasilimali hizi kwa pamoja huiwezesha Kanda kutunza, na kusambaza dawa na vifaa tiba kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na usalama.
Mafanikio ya kanda ya MSD Kilimanjaro yanatokana na uwapo wa timu ya wataalamu 38 ikihusisha wabobezi wa masuala ya ugavi ,wafamasia, wahasibu, wawakilishi wa mauzo, maofisa huduma kwa wateja, mafundi sanifu vifaa tiba na madereva. Mchango wao wa kitaalamu unahakikisha kuwa kanda hii inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa usambazaji katika maeneo yake.
Utoaji wa Huduma Bora
Kwa kuzingatia eneo lake la kimkakati, miundombinu ya kisasa, na nguvu kazi yenye ujuzi, Kanda ya MSD Kilimanjaro inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.
Kanda hii pia, inaendelea kujidhatiti kutekeleza dira kuu ya MSD ya kuwa "Kituo Bora cha Umahiri katika Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya Barani Afrika".