Kanda ya Mwanza
Kanda ya Bohari ya Dawa Mwanza ilianzishwa mwaka 1993 ikiwa na jukumu kuu la kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika mikoa ya kanda ya ziwa. Kanda hii inahudumia mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, na Simiyu, pamoja na baadhi ya wilaya za Mkoa wa Geita (Nyang’hwale, Manispaa ya Geita, na Halmashauri ya Wilaya ya Geita) kutokana na ukaribu wa eneo kijiografia na urahisi wa ugavi kutokea Mwanza.
Mawanda ya Utoaji Huduma
Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi nchini Tanzania ya mwaka 2022, Kanda ya Mwanza inahudumia jumla ya watu 12,076,371. Idadi hii inajumuisha
Mkoa wa Mwanza – watu 3,699,872,
Mkoa wa Simiyu – watu 2,140,497,
Mkoa wa Shinyanga – watu 2,241,299,
Mkoa wa Mara – watu 2,372,015,
Mkoa wa Geita – Wilaya ya Nyang’hwale- watu 225,803, Manispaa ya Geita – watu 361,671, Wilaya ya Geita – watu 1,035,214.
Kanda ya MSD Mwanza inahudumia jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 1,420, ikijumuisha vituo kuanzia ngazi ya msingi, ngazi ya kati, hadi ngazi ya taifa.
1. Vituo ngazi ya kati na taifa – Hospitali ya Rufaa ya Kanda 1, na hospitali za Rufaa za Mikoa 5.
2. Vituo ngazi ya msingi – Hospitali 31 za wilaya zilizo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – (TAMISEMI), hospitali teule 4 za Wilaya, vituo vya afya 153, na zahanati 1,207,
3. Vituo vya Tasisi za kidini na taasisi nyingine za umma - Taasisi nyingine za umma 19.
Uwezo wa Uhifadhi na Uendeshaji
Ili kuhudumia vituo vya afya ipasavyo na kwa ufanisi, kanda hii ina ghala lenye ukubwa wa eneo la mita za mraba 2,742 na magari 21 ya usambazaji yenye ukubwa tofauti kulingana na mahitaji. Rasilimali hizi kwa pamoja huiwezesha Kanda kutunza, na kusambaza dawa na vifaa tiba kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na usalama.
Mafanikio ya kanda ya MSD Mwanza yanatokana na uwapo wa timu ya wataalamu 51 ikihusisha wabobezi wa masuala ya ugavi ,wafamasia, wahasibu, wawakilishi wa mauzo, maofisa huduma kwa wateja, mafundi sanifu vifaa tiba na madereva. Mchango wao wa kitaalamu unahakikisha kuwa kanda hii inaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa usambazaji katika maeneo yake.
Utoaji wa Huduma Bora
Kwa kuzingatia eneo lake la kimkakati, miundombinu ya kisasa, na nguvu kazi yenye ujuzi, Kanda ya MSD Mwanza inaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya mikoa ya Kanda ya ziwa nchini Tanzania.
Kanda hii pia, inaendelea kujidhatiti kutekeleza dira kuu ya MSD ya kuwa "Kituo Bora cha Umahiri katika Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya Barani Afrika".