Serikali ya Misri Yatoa Msaada wa Vifaa vya Matibabu kwa Tanzania
Ubalozi wa Misri nchini Tanzania leo Septemba 8, 2022 umetoa msaada wa vifaa tiba kwa Serikali ya Tanzania ili kuboresha huduma za afya nchini.
Vifaa hivyo vyenye thamani ya dola za kimarekani elfu 27 (USD 27,000) ambazo ni sawa na takriban shilingi milioni 62.9 za kitanzania, vimekabidhiwa rasmi kwa serikali ya Tanzania.
Akikabidhi msaada huo Balozi wa Misri nchini Mhe. Mohamed Gaber Abuwafa amesema kuwa serikali ya Misri itaendelea na juhudi za kuiunga mkono serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya.
“Serikali ya Misri kupitia shirika lake la EAPD imetoa msaada huu ili kuboresha huduma za afya, ikumbukwe kuwa huu sio msaada wa kwanza na hautakuwa wa mwisho, kwani nchi zetu zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika nyanja mbalimbali, hivyo pamoja na msaada huu, tunatarajia kuanzisha ushirikiano katika siku zijazo katika kubadilishana utaalamu na wataalamu kupitia sekta ya afya”. Alisisitiza Balozi Mhe. Abuwafa
Mhe. Abuwafa ameongeza kuwa, serikali ya Misri inaangalia uwezekano wa kuwekeza nchini humo katika sekta ya dawa na vifaa vya matibabu, ili kuendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
“Serikali ya Misri itaendelea kuunga mkono sekta mbalimbali nchini ikiwemo uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza dawa ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na jamii kwa bei nafuu,” alisema Balozi Abuwafa.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Mfamasia Mkuu wa Serikali Daudi Msasi, aliishukuru Serikali ya Misri kupitia ubalozi wake nchini, kwa kuipatia Tanzania msaada huo, na kusisitiza kuwa utakuwa chachu ya kuboresha afya za wananchi wake.
“Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, tunaipongeza na kuishukuru Serikali ya Misri kwa kutupatia msaada huu ili kuboresha afya za Watanzania na ushirikiano uliopo kati ya mataifa yetu, tunatarajia huu hautakuwa msaada wa mwisho, bali ni mwendelezo wa ushirikiano zaidi kati ya mataifa yetu. Alisema Msasi