MSD Yatoa Mafunzo kwa Wataalamu wa Vifaa Tiba na Maabara Nchini.
Mafunzo ya siku tatu kwa wahandisi wa vifaa tiba na wataalam wa maabara nchini yamehitimishwa leo mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa wakati mmoja katika mikoa mitano kwa wataalam kutoka nchi nzima, yalilenga kutoa mafunzo kwa wataalam wa ufungaji, matumizi na matengenezo ya mashine na vifaa vya maabara vinavyosambazwa na MSD.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji Bw.William Singano alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wahandisi wa vifaa tiba na wataalamu wa maabara kwani yanawawezesha watumiaji kumudu kuvitumia, kuvitunza na kuvitengeneza.
Mheshimiwa Singano ameitaka Serikali kuboresha huduma za afya kwa kuwezesha mashine na vifaa vya kisasa kote nchini. Mafunzo hayo yametolewa katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro na Mwanza ambapo wataalam kutoka mikoa mingine yote walijumuika kupata mafunzo hayo.