Kamati ya Afya ya Bunge la Zambia Yaipongeza MSD kwa Maboresho ya Utendaji na Ujenzi wa Viwanda
Kamati ya Baraza la Wawakilishi la Zambia ya Afya, Maendeleo na Huduma za Jamii imefurahishwa na hatua ya Bohari ya Dawa (MSD) kuanza kuzalisha baadhi ya bidhaa za afya kwa kutumia wataalamu wake wa ndani.
Hayo yamesemwa leo tarehe 26/5/2022 baada ya Kamati ya Afya kutoka Zambia kutembelea MSD kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala yanayohusu ugavi wa bidhaa za afya.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe hao, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya, Maendeleo na Huduma za Jamii ya Baraza la Wawakilishi la Zambia Mhe. Dk.Christopher K. Kalila alisema wamefurahishwa na hatua ya Bohari ya Dawa (MSD) kuanza kuzalisha baadhi ya bidhaa za afya kwa kutumia wataalamu wake wa ndani.
Mhe. Dk Kalila aliongeza kuwa MSD Tanzania ni sawa na pacha wa Bohari ya Dawa nchini Zambia, kwani sheria yao pia imefanyiwa marekebisho ili kuiwezesha Bohari hiyo kuanza kuzalisha bidhaa za afya.
“Ni vyema taasisi zetu mbili zikakaribia kubadilishana uzoefu na utaalamu katika maeneo mbalimbali ili kwa pamoja kusukuma ajenda ya uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za afya na kuondoa utegemezi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi sambamba na kupunguza gharama,” alisema Dk Kalila.