Dk.Mollel akiishauri MSD namna ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Naibu Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel ameishauri Wakala wa Dawa Tanzania (MSD) kuandaa mpango wa muda mrefu wa kuzungumza na watengenezaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya kutoka nchi zinazozalisha bidhaa hizo, kuja kuwekeza nchini Tanzania, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Naibu Waziri ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Wadau wa Bidhaa za Afya Afrika Mashariki yaliyoanza leo jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa MSD pia iangalie namna ya kuingia mikataba na nchi zinazozalisha bidhaa za afya ili kurahisisha ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwao, ili kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa zinazokidhi mahitaji.
Kiongozi huyo pia aliwahimiza wazalishaji hao wa kigeni kuja kuwekeza Tanzania kwa kuingia ubia na serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa MSD Bi Etty Kusiluka alimshukuru Dk.Mollel kwa ushauri huo na kuahidi kuufikisha kwa Menejimenti ya MSD ili uweze kufanyiwa kazi.
Aidha, aliendelea kuwaalika wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda la MSD kwenye maonesho hayo, ili waweze kupata taarifa mbalimbali zinazohusu MSD, sambamba na kufahamu namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
Maonyesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Afya ya Afrika Mashariki yanafanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, uliopo jijini Dar es Salaam, yakiwakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali.