Bohari ya Dawa ya Msumbiji Yapongeza Juhudi za MSD za Kuboresha Huduma, Ikiwemo Ujenzi wa Viwanda
Ujumbe kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa vya Msumbiji (ANARME) leo umetembelea Makao Makuu ya MSD kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Ujumbe wa Msumbiji ulitembelea maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya za MSD pamoja na kiwanda cha kuzalisha barakoa na kiwanda cha kutengeneza tembe za KPI.
Wajumbe hao walifurahishwa na hatua ya MSD kuongeza nafasi yake katika kuzalisha bidhaa za afya jambo ambalo linasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Aidha, pamoja na mambo mengine, ujumbe huo ulikutana na Kurugenzi za Ugavi na Tehama na kupata maelezo ya namna mifumo mbalimbali inavyofanya kazi katika mnyororo wa ugavi na kuahidi kuiga kanuni bora mara watakaporejea nchini kwao.
Katika hatua nyingine, ujumbe huo ulipata fursa ya kuwatembelea wateja wa MSD ambao ni Hospitali ya Mifupa, MOI na Taasisi ya Moyo (JKCI) kwa lengo la kujifunza namna taasisi hizo zinavyofanya kazi.