Serikali Inaendelea Kusaidia Ujenzi wa Viwanda vya MSD vya Dawa na Vifaa Tiba.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu, leo amezindua Bodi mpya ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) na kuwaagiza wajumbe wa Bodi hiyo kuhakikisha wanawezesha uboreshaji wa upatikanaji wa bidhaa bora za afya na nafuu.
Waziri Ummy aliwaeleza wajumbe wa Bodi kuwa watapimwa kwa kuangalia hali halisi ya upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Pia alisisitiza kuwa wanahakikisha katika majukumu yote ya MSD wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zote za manunuzi ya umma, ili kuleta ufanisi na tija katika utendaji kazi, sambamba na kuondoa masuala ya ukaguzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Bi Rosemary Silaa amewataka watumishi wa MSD kubadilika na kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kubadilisha taswira inayojengeka katika utendaji usioridhisha wa taasisi hiyo.
Wajumbe hao ni pamoja na Bi Rosemary Silaa ambaye ni Mwenyekiti, Dk Julius Mwaiselage, Dk.Ntuli Kapologwe, Meshack Anyingisye, Rehema Katuga, John Mathew Mnali, Dk.Mwamvita Kissiwa, Dk.Danstan Hipolite Shewiyo na Brenda Msangi.