SADC Yazindua Kanzidata ya Mfumo wa Taarifa za Bidhaa za Afya Kwa Nchi Wanachama
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezindua kanzidata maalum kwa ajili ya ukusanyaji na usindikaji wa taarifa za dawa na vifaa tiba kutoka kwa wazalishaji na wauzaji mbalimbali duniani, ambapo mfumo huo utarahisisha upatikanaji na ununuzi wa bidhaa za afya kutoka nchi wanachama.
Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 14/05/2024 jijini Dar es Salaam, na kushuhudiwa na Bohari za Dawa za nchi za SADC, pamoja na viongozi mbalimbali wa Sekta ya Afya wa jumuiya hiyo, waliokutana kwa siku mbili jijini humo.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt John Jingu amesema kupitia mfumo huo nchi wanachama zitaweza kupata taarifa za kina za dawa na vifaa tiba mfano mahali zinapatikana au kutengenezwa bei yake pamoja na kujua tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa husika.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inasaidia kufikia malengo ya Wakuu wa Nchi za SADC kuwa na mfumo wa pamoja wa ununuzi wa bidhaa za afya kwa sababu wanaponunua kwa pamoja hupunguza gharama, pia huongeza nguvu ya ushawishi na kuvutia wawekezaji kufungua viwanda vya dawa na vifaa tiba ndani ya nchi za SADC.
"Mfumo huu ni nyenzo muhimu katika sekta ya afya ili kukuza ushirikiano kati ya nchi za SADC katika afya ya watu wetu, hivyo dawa na vifaa tiba ni muhimu katika kulinda afya ya binadamu," alisema Dk. Jingu.
Kwa upande wake mwakilishi wa sekretarieti ya SADC Calicious Tutalife alisema kupitia mfumo huo SADC itaweza kubadilishana taarifa muhimu hasa za manunuzi ya pamoja na kufanya maamuzi ya bidhaa zipi zinunuliwe ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.
Aidha alisema watatumia mfumo huo kupata bidhaa bora na za bei nafuu kupitia taarifa watakazozipata kwenye mfumo huo na kuandaa mpango ambao watasimamia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania, Tukai Mavere, alisema kuwa takwimu hizo zitatumika kuhifadhi taarifa za bidhaa za afya, nchi zinakotoka, ubora wake, gharama zake, jambo ambalo litasaidia wananchi kujua jinsi nchi mbalimbali zinavyopata bidhaa na bei.
Hata hivyo alisema ili kuhakikisha ufanisi utaundwa kitengo maalum cha pamoja kitakachokuwa na bodi ya usimamizi kutoka nchi wanachama kwani jukumu hilo ni la kimataifa.
Aliongeza kuwa kwa sasa MSD kwa kushirikiana na Sekretarieti ya SADC watafanya mapitio ya bidhaa za afya zinazohitajika, na wataangalia sheria, miongozo, pamoja na kupata vibali vyote vya serikali kwa nchi wanachama, kwani ni maeneo muhimu katika kutekeleza manunuzi ya pamoja.
Itakumbukwa kuwa Tanzania ndiyo nchi iliyochaguliwa na SADC kutekeleza jukumu la Ununuzi wa Pamoja wa dawa na vifaa tiba kwa nchi zote za SADC kupitia MSD, kutokana na Tanzania kuonekana kufanya vizuri katika eneo hilo.