Skip to main content
MSD Planning, Monitoring and Evaluation Manager, Hassan Ally Ibrahim Speaking to Journalists, Recently at the Mawezi Media Center in Dodoma

MSD Yabainisha Mikakati Yake kwa Mwaka 2023/2024

Bohari ya Dawa (MSD) imebainisha kwamba katika Mwaka wa Fedha 2023/24, inatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya zikiwemo dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kupitia mikakati maalumu iliyowekwa na Bohari hiyo.

Mikakati hiyo imeelezwa leo na Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ally Ibrahim katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maboresho ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwa ni mwendelezo wa Taasisi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, kitakachofanyika cha kwanza ni kuhimiza matumizi ya takwimu ili kufahamu mahitaji, wakati na maeneo ambayo bidhaa za afya zinahitajika, maeneo mengine ya msingi ambayo kwa sasa MSD inayafanyia kazi ni kuimarisha mfumo mzima wa ununuzi kwa kuangalia vizuri mikataba ili bidhaa za afya zisikosekane”.

“Vilevle, tutahimiza ushirikiano na wazalishaji wa ndani ambapo tutatoa fursa kwa kuzingatia misingi ya kisheria na kununua bidhaa kutoka kwao,” amesema Meneja Ibrahim.

Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na miundombinu ya utunzaji wake kupitia fedha zitakazotolewa na Serikali, kuanza uzalishaji wa mipira ya mikono kwa kiwanda kilichopo katika Kijiji cha Idofi, mkoani Njombe ambacho kipo mbioni kukamilika, kuanza kutekeleza miradi ya uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya eneo la Zegereni, mkoani Pwani na uanzishaji wa viwanda vya Pamba tiba.

Mikakati mingine ni pamoja na  maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa pamoja na bidhaa za pamba tiba na kuanza ujenzi wa maghala ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Kagera kwa lengo la kuongeza nafasi za kuhifadhi bidhaa na kuimarisha ubora wa bidhaa za afya, ambapo ujenzi wa maghala hayo unatarajiwa kuanza mwezi Agosti 2023.

Utekelezaji wa majukumu hayo ya MSD unaenda sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya maboresho ya utendaji yaliyotolewa na Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, wakati alipoteua uongozi mpya wa Bohari hiyo.

Ameongeza kuwa MSD inapitia mifumo yote ya uendeshaji ikiwemo mnyororo wa ugavi, usimamizi na TEHAMA ili kuendana na kasi ya ongezeko la ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, vinavyojengwa na Serikali na kuhakikisha malengo ya Serikali katika upatikanaji wa bidhaa za afya yanafikiwa.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.