MSD yatambuliwa kwa kushiriki na kudhamini kongamano la nne la kitaifa la ufuatiliaji, tathimini na kujifunza
Baadhi ya watumishi wa Bohari ya Dawa (MSD) wameshiriki katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza (MEL) linalofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 10 hadi 13 Septemba, 2025. Kongamano hili ambalo limeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu (PMO-PPC), limepambwa kwa kaulimbiu isemayo “Community-Led M&E: Building Local Capacity and MEL Ownership” ikisisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika mchakato wa ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kujenga uwezo wa ndani na kumiliki mifumo hiyo kwa ngazi ya jamii.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, huku kilele cha kongamano hilo kikifungwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dotto Mashaka Biteko. Katika kongamano hilo, MSD imetambuliwa kwa kuwa mmoja wa wadhamini wa tukio hilo muhimu, ikiwa ni ishara ya mchango wake mkubwa katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini nchini.
Ushiriki wa MSD umetoa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuonesha mchango wake katika kuimarisha huduma za afya kupitia mifumo madhubuti ya M&E. Kongamano hili limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, taasisi za kiraia, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wawakilishi wa jamii kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa miradi na huduma kwa kutumia ushahidi na takwimu za M&E.