Bohari ya Dawa (MSD) imekutana na wateja wake wakubwa
Bohari ya Dawa (MSD) imekutana na wateja wake wakubwa (Corporate customers) jijini Dodoma kutathimini, kuupitia na kuuboresha mkataba unaotumiwa na MSD kuwahudumia wateja wakubwa. Pamoja na kupitia mkataba huo wateja hao wamepata wasaa wa kuwasilisha maoni mbalimbali kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma kutoka MSD.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Ugavi, Meneja Huduma kwa Wateja Gendi Machumani, amesema baada ya muongozo huo kukamilika utaratibu mzima wa kuhudumia wateja wakubwa utaainishwa.
Bi. Machumani ameeleza kuwa MSD imeendelea kuhakikisha inakidhi mahitaji ya wateja wakubwa ambao wengi wao wanakuwa na mahitaji maalumu ambapo hadi sasa MSD ina takribani wateja wakubwa 45 nchi nzima.
Kwa upande wake Msimamizi wa wateja wakubwa wa MSD ndugu Michael Bajile amesema vikao kama hivyo kwa wateja wakubwa vinaendelea ili kuendeleza majadiliano ya wazi, yenye lengo la kuimarisha huduma. “Vikao hivi vitakuwa na muendelezo, tukiamini kuwa majadiliano ya wazi na ya mara kwa mara na wadau wetu ni nyenzo muhimu ya kufanikisha lengo letu la kuwa kitovu cha ugavi wa bidhaa bora za afya nchini,”alisisitiza Bajile .