Bohari ya Dawa (MSD) imekuwa ikihudumia vituo vya umma vya kutolea huduma za afya nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 30, na inaendelea kubuni na kudumisha mifumo yenye ufanisi, usalama, na gharama nafuu katika majukumu yake makuu manne za Uzalishaji, Ununuzi, Uhifadhi, na Usambazaji wa bidhaa za afya kwa vituo vyote vya afya vya umma na vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
MSD imejipanga kuendelea kuhakikisha inatimiza mahitaji yote ya vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo dawa, vifaa vya kisasa vya kiuchunguzi na vifaa tiba vinginevyo kwa kutumia wataalamu mbalimbali waliopo katika sekta ya afya. Matarajio ni kwamba uwekezaji kwenye eneo la TEHAMA utsaidia kufanya utambuzi wa mahitaji ya wateja na kuweza kufikia matarajio ya utoaji huduma kwa wadau wote hivyo kuifanya MSD kuwa stahamilivu na kujiendesha kwa ufanisi.
Kama mdau muhimu katika sekta ya afya, MSD inaendelea kujipanga upya kwa kufanya maboresho ya utendaji wake, na kukabiliana na mahitaji pamoja na matarajio yanayoibuka kutoka kwa wadau mbalimbali. Maeneo ya kipaumbele katika mabadiliko haya, ni pamoja na kuongeza na kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya, kuimarisha utendaji, na kupunguza bei ya bidhaa kupitia mkakati maalum wa kutafuta washitiri na kuzingatia miongozo.
Kwa muktadha huo, MSD inakusudia kuimarisha uwezo wake wa kibiashara kupitia ushirika katika mnyororo wa ugavi, uzalisaji wa bidhaa za afya, tafiti, na teknolojia ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini. Shughuli zote hizi zinalenga kutimiza adhima yake ya kuwa "Kituo cha mfano wa kuigwa, katika mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya barani Afrika".