Miradi Misonge
Miradi Msonge (Vertical Programs) ni mipango inayolenga magonjwa au kundi fulani la magonjwa. Mwanzoni mwa miaka ya 1980 hadi 1990 programu mbalimbali kama vile Mpango wa Afya ya Uzazi, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Mpango wa Taifa wa Chanjo, Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma ilikuwa chini ya Wizara ya Afya. Kila mradi ulikuwa unafanya kazi kivyake ikiwepo shughuli za usambazaji. Matokeo ya utafiti katika sekta ya afya yalionyesha uendeshaji wa kila mradi kwa kujitegemea kulingana na kazi zake za ugavi ilikuwa ghali na hivyo kupoteza rasilimali. Hivyo, ili kuboresha ufanisi katika sekta ya afya mwaka 1996, Serikali ilijumuisha kazi zote za ugavi wa miradi misonge ndani ya shughuli za MSD, na kazi zilizounganishwa zilikuwa kama ifuatavyo:-
a.Uratibu wa ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa dawa za miradi, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara;
b.Kusimamia upokeaji wa dawa zote, vifaa vya matibabu na vitendanishi vya maabara vinavyotolewa na
programu tofauti na Washirika wa Maendeleo (Global Fund, UNICEF, Shirika la Afya Duniani na USAID);
c.Kutoa ripoti kwa wakati kwa miradi na washirika wa maendeleo juu ya hali ya upatikanaji wa bidhaa
ghalani (stock status).
Ujumuishaji wa huduma za Miradi Msonge ndani ya MSD umeimarisha huduma za Miradi hiyo na kupunguza gharama za uendeshaji wake. Hatua hii imeongeza upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vya afya. Kwa sasa MSD inafanya kazi na Programu tofauti chini ya Wizara ya Afya na washirika wa maendeleo wanaochangia mipango ya afya nchini. Programu hizo ni pamoja na:- Mpango wa Afya ya Uzazi, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Mpango wa Taifa wa Chanjo, Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma, Mpango wa Magonjwa ya Kitropiki Yaliyosahaulika, Mpango wa Taifa wa Malaria, Mpango wa Chakula na Lishe Tanzania, Mpango wa Meno na nyinginezo. Kwa upande mwingine, MSD hupokea bidhaa za afya chini ya msaada kutoka kwa washirika mbalimbali wa maendeleo kama vile: - Global Fund, UNICEF, WHO na USAID. Washirika wote huleta bidhaa mahususi za afya ili kuongeza bidhaa za afya kwa Serikali au usaidizi wa moja kwa moja katika masuala ya rasilimali fedha kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa zitakazowasilishwa kwenye vituo. Dawa zote za Miradi Misonge, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara huwasilishwa kwenye Kanda za MSD na vifaa vyote kupitia mifumo tofauti kama ilivyodadavuliwa hapa chini:- a. Usambazaji wa moja kwa moja kwenye Wilaya na Mikoa chini ya mfumo wa Push System kadiri inavyoelekezwa na Programu (Kinga na Mpango wa Kifua Kikuu na Ukoma); b.Usambazaji kulingana na kampeni maalum za kushughulikia changamoto mahususi (Neglected Tropical Diseases, Tanzania Food and Nutrition Centre, chanjo, Dengue); c.Usambazaji kupitia mfumo wa Smart Push. Kanda za MSD hukusanya na kupokea mahitaji ya vituo na kuyawasilisha Makao Makuu kila mwezi kwa ajili ya kupelekewa huduma. Bidhaa za miradi msonge zote zimeunganishwa na mfumo wa uagizaji na usambazaji kwa mujibu wa kalenda ya usambazaji ya MSD.