Tunafanya nini
Bohari ya Dawa (MSD) ni idara inayojitegemea chini ya Wizara ya Afya (MoH), iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa Sheria ya Bohari ya Dawa, Sura. 70.Mwaka 2020 sheria ya MSD ilifanyiwa marekebisho na kuifanya MSD kuwa na majukumu makuu manne ambayo ni Uzalishaji, Ununuzi, Uhifadhi na Usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya umma zaidi ya 7,600 nchi nzim na baadhi vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Hivyo MSD inajukumu la kuandaa, kutunza na kusimamia mfumo bora na wa gharama nafuu za ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba vinavyohitajika kwa matumizi ya vituo vyote vya afya vya umma. Karibu asilimia 85 ya bidhaa zote za afya za MSD zinanunuliwa kutoka nje ya nchi.
Bohari ya Dawa ina Kanda kumi (10) ambazo zimewekwa kimkakati. Kanda hizo ni pamoja na Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Tabora, Dodoma, Kagera, Mwanza, Kilimanjaro, Tanga na Mtwara. Halikadhalika, MSD inaendesha Maduka Matano (5) ya kijamii yaliyokusudiwa kusogeza huduma za bidhaa za afya kuwa karibu na jamii.
Maduka haya yanapatikana katika maeneo yafuatayo; Geita (Chato), Lindi (Ruangwa), Katavi (Mpanda), Arusha (Mlima Meru), na Mbeya. MSD inasambaza bidhaa za afya moja kwa moja kwenye vituo vya afya na usambazaji huu hufanyika kila baada ya miezi miwili.
Kanda za MSD husambaza bidhaa za afya moja kwa moja hadi kwa mteja, na kukabidhi bidhaa hizo, mbele ya Kamati ya Afya ya kituo husika. Usambazaji huo hufanyika kila baada ya miezi miwili kwa kufuata kalenda ya usambazaji.