Kamati ya Bunge ya Afya na UKIMWI, Yaridhishwa na Utekelezaji wa Mradi wa Gloves - MSD Idofi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, yaeleza kuridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi wa Kiwanda cha kuzalisha Mipira ya Mikono cha MSD, kilichoko idofi, Makambako Mkoani Njombe.
Hayo yameelezwa agosti 7, 2024 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe.Christina Mnzava, wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo kwa lengo la kukagua na kupokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.
Mhe. Mnzava kwaniaba ya kamati hiyo, amepongeza juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na MSD, katika kuendeleza mradi huo, ambayo umetoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo.
Aidha, kamati hiyo imeitaka MSD kuhakikisha inakuja na mpango na mkakati madhubuti wa kufunga mashine za viwanda vingine vya Dawa, zilizoko eneo hilo, ili kutimiza adhima ya serikali ya kuletwa kwa mashine hizo.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwaniaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meneja Mipango, Tathimini na Ufuatiliaji wa MSD Hassan Ally, ameeleza kwamba Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha glavu milioni 80 kwa mwaka, ukilinganisha na mahitaji ya nchi ya milioni 58 kwa mwaka, ambayo hugharimu takribani bilioni 16.7.
Ameongeza kwamba hadi kufikia Juni 2024, uwekezaji Kiwandani hapo umefikia jumla ya bilioni 12.4, ambazo ni gharama za uwekezaji na Uendeshaji kwa mwaka wa kwanza.
Aidha amesisitiza kwamba katika kipindi cha miezi 5 kiwanda hicho kimezalisha jumla ya gloves milioni 4, zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.14, ambazo zimeanza kuingia sokoni mwezi Agosti 2024.
Naye Naibu waziri wa Afya, Mhe. Godwin Mollel, ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa inaoendelea kuufanya kwenye sekta ya Afya, ikiwemo uanzishwaji wa viwanda.
Aidha, amebainisha maendeleo yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi cha utawala wake, huku akisisitiza kwamba serikali itaendelea kuhakikisha miradi yote inatekelezwa.