Skip to main content
Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango, akimpatia nyaraka mbalimbali, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae kilichopo Lushoto mkoani Tanga,

MSD Yakabidhi Vifaa Tiba vya Mil. 114 - Kituo cha Afya Mtae

SERIKALI imetoa Sh.Milioni 114 kwa Kituo cha Afya  Mtae kilichopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambazo zimetumika kununulia vifaa tiba kupitia Bohari ya Dawa (MSD) na hivyo kinatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji mwishoni mwa mwezi Disemba 2023.

Hatua ya kituo hicho kuanza  kutoa huduma hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya kuibadilisha zahanati ya kijiji cha Mtae kuwa Kituo cha  Afya ili wananchi waweze kupata huduma bora na karibu.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,  Shafii Makamba akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo kutoka MSD alianza kwa kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani kupitia MSD kwa kuwezesha kutoa vifaa hivyo vya dharura kwa ajili ya kufanya huduma ya dharura kwa wakina mama na watoto.

"Vifaa hivi tulivyovipokea leo kutoka MSD Kanda ya Tanga  vitasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwa sababu kabla ya hapo walikuwa wakilazimika kutembea umbali usiopungua kilometa 65 kwenda Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kupata huduma za dharura hasa za upasuaji na kuwa wataachana na adha hiyo na kupata huduma hii hapa hapa katika kituo chetu," alisema Makamba.

Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Tanga, Mary Isango akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Sitti Abdulrahman, alisema wamepeleka vifaa hivyo baada ya kituo hicho cha afya kujengwa jengo la upasuaji na kupelekewa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh.Milioni 114 ambavyo vinaenda kuondoa changamoto waliyokuwa wakiipata wananchi kwenda kupata huduma hiyo mbali.

"Huduma za upasuaji sasa zitafanyika katika kituo hiki baada ya kupata vifaa hivi ambavyo ni muhimu sana sisi kama bohari ya dawa wito wetu kwa watendaji wa kituo hiki ni kuvitunza ili viweze kudumu muda mrefu na kuleta tija kwa wananchi kadri watakavyokuwa wakiendelea kuvitumia kwa kuzingatia kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua," alisema Isango.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mtae, Beatrice Alphonce, Disifa Mdoe na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Andrew Kilama waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vitaondoa kabisa madhira waliyokuwa wakiyapata na wakati mwingine kusababisha vifo.

"Tulikuwa na changamoto kubwa baadhi ya wajawazito walikuwa wakijifungulia njiani kutokana na umbali mrefu wa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kupata huduma lakini sasa tutakuwa tunaipata hapahapa nyumbani kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu mama Samia kwa kutuona na kutuonea huruma wanawake wenzake na kama ingewezekana tungemuomba siku moja aje hayaone kwa macho maendeleo haya aliyotuletea," alisema Alphonce.

Alphonce alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia, Mbunge wa jimbo hilo, Rashid Shangazi na viongozi wa wilaya hiyo kwa jitihada kubwa wanayoifanya ya kuwaletea maendeleo hayo ambapo aliwaombea kwa Mungu awape afya na maisha marefu.

 

About MSD

Medical Stores Department (MSD) was established by the Act of Parliament No.13 of 1993 as an autonomous department under the Ministry of Health, Community Development, Gender, Elderly and Children responsible for developing, maintaining and managing an efficient and cost effective system of procurement, storage and distribution of approved medicines and medical supplies required for use by all public health facilities.