Wizara ya Afya Yaridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi wa Ghala la MSD Chato.
Wizara ya Afya imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ghala jipya la kuhifadhia bidhaa za afya la Bohari ya Dawa (MSD) linalojengwa wilayani Chato, Mkoani Geita, ambao utekelezaji wa mradi huo umefikia 65%. Hali hiyo inayotokana na kasi ya ujenzi unaozingatia viwango na kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa, hatua inayoweka mazingira mazuri ya kukamilika kwa mradi huo kwa wakati.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Programu ya Uimarishaji wa Mifumo ya Afya iliyo Stahimilivu na Endelevu (RSSH), kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Hussein Athumani, alipofanya ziara maalum ya kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, ili kupima mwenendo wa ujenzi na kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na mipango ya mradi chini ya programu ya Global Fund RSSH.
Dkt. Hussein Athumani alisema Wizara ya Afya inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa kupitia ufadhili wa Global Fund, ili kuhakikisha inazingatia viwango vya ubora, na kukamilika kwa wakati ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa kuimarisha sekta ya afya nchini.
Aidha, ziara hiyo ilitoa fursa ya kubaini changamoto au vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa mradi na kujadiliana na timu ya utekelezaji, kuhusu hatua za udhibiti, ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa. Kupitia Ziara hiyo, ilibainika kuwa sehemu kubwa ya kazi za msingi na miundombinu ya jengo zimekamilika, huku hatua za umaliziaji (finishing works) zikiendelea ili kuendana na kalenda ya ukamilishaji wa mradi, iliyoainishwa awali kwa mujibu wa mkataba.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa rasmi tarehe 19 Oktoba, 2026, ndani ya kipindi cha utekelezaji wa mradi wa Global Fund Cycle 7, huku ukitarajiwa kuongeza uwezo wa MSD wa kuhifadhi bidhaa za afya, kuboresha usimamizi wa bidhaa hizo na kuimarisha ufanisi wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini. Hatua hiyo itaongeza upatikanaji endelevu wa huduma za afya kwa wananchi na kuchangia ujenzi wa mfumo wa afya ulio imara, stahimilivu na endelevu.