Ruka kwenda maudhui makuu

Tanzania Yajipanga Kuwa Kitovu cha Uzalishaji wa Dawa Afrika, Yawaalika Wawekezaji wa China

Serikali ya Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kujenga sekta imara ya viwanda vya dawa na kuifanya nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko barani Afrika, huku ikizidi kuvutia uwekezaji wa kimkakati kutoka China.

Akizungumza leo  Julai 7,2026 katika kikao na viongozi wa kampuni ya Jointown Pharmaceutical Group nchini China, inayoongoza kwa uzalishaji wa madawa kwa upande wa makampuni binafsi nchini hapa, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Tanzania imejipanga kuendeleza Eneo Maalum la Kiuchumi la Dawa na Vifaa Tiba la Mloganzila, ambalo litakuwa kitovu cha uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, malighafi za dawa (APIs) na vifaa tiba.

Amesema, eneo hilo limeboreshwa kwa miundombinu ya kisasa na linaunganishwa kwa urahisi na Bandari ya Dar es Salaam pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na Jointown katika kuanzisha uzalishaji wa malighafi za dawa, hatua itakayoongeza uwezo wa Tanzania kujitosheleza kwa dawa muhimu na kuiwezesha kuhudumia masoko ya kikanda.

“Ushirikiano kati ya Jointown na Bohari ya Dawa (MSD) unatarajiwa kuleta mageuzi katika mifumo ya ugavi, uhifadhi na usambazaji wa dawa nchini kupitia matumizi ya teknolojia na uzoefu wa kampuni hii kubwa hapa China katika usimamizi wa minyororo ya usambazaji duniani” amesema Mhe. Mchengerwa

Aidha Mhe. Mchengerwa amethibitisha Serikali inayoongozwa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inafuatilia kwa karibu uwekezaji wa dawa nchini na ameahidi ushirikiano wa Serikali kwa wawekezaji watakaochangia maendeleo ya sekta ya afya.

Katika kuonesha utayari wa Serikali, Waziri Mchengerwa amesema Tanzania ipo tayari kutenga maeneo ya kutosha  kwa ajili ya uwekezaji wa uzalishaji wa malighafi za dawa, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya dhati ya kuharakisha uanzishwaji wa viwanda vya kisasa vitakavyozalisha dawa kwa matumizi ya ndani na kwa ajili ya soko la Afrika.

Katika ziara yake, Waziri Mchengerwa ameongozana na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaatiba Emmanuel Tayari, Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba TMDA Prof. Adam Fimbo, pamoja na watendaji wengineo wa Wizara ya Afya na Taasisi zilizo kwenye mnyororo wa ugavi wa Bidhaa za Afya nchini.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.