Ruka kwenda maudhui makuu

Mwenyekit Bodi ya Wadhamini MSD, Aridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi wa Ghala la MSD-CHATO

Chato, Geita 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD), Bi. Rosemary Silaa, ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa ghala jipya la kisasa la MSD linalojengwa wilayani Chato mkoani Geita, huku akimtaka mkandarasi Kampuni ya Hainan International kuhakikisha anazingatia ubora uliokusudiwa na kukamilisha mradi huo ndani ya muda wa mkataba.

Akizungumza Mei 15, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Bi. Silaa alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa MSD wa kuimarisha na kupanua mtandao wa uhifadhi na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa za afya nchini, ili kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.

“Tumefurahishwa na hatua iliyofikiwa, lakini ni muhimu mkandarasi kuhakikisha ubora wa kazi unazingatiwa kwa viwango vilivyokusudiwa na mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba. Hili ni eneo muhimu sana kwa ustawi wa huduma za afya nchini,” alisema Bi. Silaa.

Bi. Silaa aliongeza kuwa ujenzi wa ghala hilo la kisasa lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800 utakuwa chachu kubwa ya kuboresha usambazaji wa bidhaa za afya hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambayo inahudumiwa na vituo vingi vya kutolea huduma za afya.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, hadi sasa ujenzi wa jengo la ghala umefikia asilimia 42, wakati jengo la ofisi limefikia asilimia 58. Aidha, kazi za nje (external works) ikiwemo ukuta wa uzio, jengo la ulinzi, jengo la jenereta, banda la taka na kisima cha maji, zimefikia asilimia 46 ya utekelezaji wake.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu, na baada ya kukamilika kwake utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine muhimu katika vituo vya afya vya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Bi. Silaa alibainisha kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya MSD ya kuimarisha miundombinu ya ugavi nchini, ili kuhakikisha huduma za afya zinakuwa za uhakika, endelevu na zenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

“Kukamilika kwa mradi huu kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya, kupunguza ucheleweshaji wa usambazaji, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisisitiza.

MSD inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati nchini yenye lengo la kuimarisha mfumo wa ugavi wa dawa na vifaa tiba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia Watanzania wote kwa wakati.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.