MSD na Rwanda Wajadili Ushirikiano Katika Ugavi wa Bidhaa za Afya
Bohari ya Dawa (MSD) imeketi mezani na ujumbe wa wataalam kutoka ‘Rwanda Medical Supply’ (RMS) kwa ajili ya kupeana uzoefu wa kiutendaji na kujadili fursa za ushirikiano katika ugavi wa bidhaa za afya, ikiwemo uzallishaji, ununuzi, uhifadhi, na usambazaji wa bidhaa za afya.
Akizungumza wakati wa kikao kilichofanyika Mei 14, 2026 katika ofisi za MSD Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya maboresho makubwa ya mifumo ya ugavi wa bidhaa za afya sambamba na kuwekeza katika uzalishaji wa ndani ili kuhakikisha kuna upatikanaji endelevu wa bidhaa bora za afya, salama na kwa wakati.
Aidha, amesema MSD iko tayari kushirikiana na Rwanda katika maeneo mbalimbali ya biashara na huduma za bidhaa za afya, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuhudumia soko la Rwanda kupitia uwezo wa MSD katika uzalishaji na usambazaji.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Rwanda Medical Supply (RMS), Dkt. Erick Nyirimigabo, amepongeza mifumo ya uendeshaji ya MSD na kueleza kuwa ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini Rwanda na kufungua fursa za ushirikiano zaidi na MSD.
Ujumbe huo pia ulipata fursa ya kutembelea Ghala Kuu la MSD Dodoma na kujionea namna MSD inavyotekeleza majukumu yake ya msingi katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.