Ruka kwenda maudhui makuu

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Aipongeza MSD, Atoa Wito wa Kuwashirikisha Wabunifu wa Ndani Kuimairisha Sekta ya Afya

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, leo ametembelea banda la Bohari ya Dawa (MSD) katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amepongeza juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine muhimu za afya nchini, sambamba na kutoa maelekezo ya kuimarisha ushirikiano na wabunifu wa ndani ili kuongeza thamani ya mnyororo wa bidhaa za afya.

Akiwa katika banda la MSD, Dkt. Magembe alipata fursa ya kutembelea na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, pamoja na ubunifu unaotumika katika kuboresha mifumo ya ugavi wa dawa na vifaa tiba nchini. Alielezwa kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa ugavi, pamoja na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kupitia upatikanaji wa bidhaa hizo kwa wakati.

Katika maelekezo yake, Dkt. Magembe aliitaka MSD kuendelea kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kukuza uchumi wa viwanda na ubunifu kwa kuwapa nafasi wabunifu wa ndani kushiriki katika kubuni na kuendeleza suluhisho mbalimbali vinavyoweza kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.

Alisisitiza kuwa Tanzania ina kundi kubwa la vijana wenye ubunifu na uwezo mkubwa wa kutengeneza teknolojia na bidhaa zinazoweza kutumika katika sekta ya afya, hivyo ni muhimu taasisi za umma kuwatambua, kuwajengea uwezo na kuwapatia fursa za kushirikiana nazo ili kuleta tija kwa taifa.

Nitawaletea vijana wabunifu mzungumze nao ili kuona kama wanaweza kupatiwa fursa ya kushirikisha MSD ubunifu wao,” alisema Dkt. Magembe.

Alieleza kuwa hatua hiyo itaongeza thamani katika mnyororo wa bidhaa za afya, kuchochea matumizi ya teknolojia za ndani, kuimarisha ushindani wa wabunifu wa Kitanzania na wakati huo huo kuchangia utekelezaji wa sera za Serikali zinazolenga kukuza ubunifu, ajira kwa vijana na maendeleo ya viwanda vya ndani.

Aidha, Dkt. Magembe alibainisha kuwa ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na wabunifu wa ndani utasaidia kupatikana kwa suluhisho zinazozingatia mazingira na mahitaji halisi ya wananchi, huku ukichochea ukuaji wa sekta ya afya kupitia matumizi ya teknolojia na maarifa yanayozalishwa nchini.

Kwa upande wake, uongozi wa MSD ulimhakikishia Katibu Mkuu kuwa taasisi hiyo itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo wabunifu wa ndani, ili kuboresha huduma zake na kuongeza ufanisi katika usambazaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya.

MSD imeendelea kutumia Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kama jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio yake, kuelimisha wananchi kuhusu majukumu yake ya msingi katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali katika sekta ya afya.

Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yamewakutanisha taasisi za umma na binafsi, wazalishaji, wabunifu na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, yakitoa fursa ya kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia mpya na kujenga ushirikiano unaochochea maendeleo ya uchumi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.