Baraza la Wafanyakazi la MSD Laweka Mkazo Kuimarisha Upatikanaji wa Bidhaa za Afya Nchini na Kuimarisha Utendaji wa Taasisi.
Bohari ya Dawa (MSD) imehitimisha kikao chake cha 27 cha Baraza la Wafanyakazi kwa kuweka maazimio na mikakati mbalimbali inayolenga kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na wadau wa sekta ya afya nchini.
Kikao hicho cha siku mbili kilifunguliwa na kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Mavere Tukai, mkoani Dodoma, ambapo viongozi na wawakilishi wa watumishi walijadili kwa kina maendeleo ya taasisi, changamoto zilizopo pamoja na mwelekeo wa utekelezaji wa vipaumbele vya kimkakati vya MSD.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao hicho, Bw. Tukai aliwapongeza watumishi wa MSD kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kujituma, hali ambayo imeiwezesha taasisi kuendelea kufikia malengo yake ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wananchi kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Mafanikio ya MSD yanatokana na mshikamano, uwajibikaji na moyo wa kujitolea wa watumishi wetu. Tunapaswa kuendelea kuzingatia maadili ya kazi, ubunifu na matumizi sahihi ya rasilimali ili kuongeza tija na kuimarisha huduma kwa wananchi,” amesema Bw. Tukai.
Katika kikao hicho, Baraza la Wafanyakazi limeweka mkazo katika kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya (stock availability) nchini kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya usambazaji, uhifadhi na usimamizi wa bidhaa hizo katika ngazi zote za huduma za afya.
Nguzo za Kimkakati Zilizopitishwa na Baraza
1. Kuimarisha Upatikanaji wa Bidhaa za Afya
Baraza limeelekeza nguvu katika kuhakikisha MSD inaendelea kuwa mhimili mkuu wa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya kwa wakati, hatua inayolenga kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na kupunguza changamoto za upungufu wa bidhaa muhimu hospitalini na vituo vya afya.
2. Urejeshaji wa Madeni ya Serikali
Kikao hicho pia kimejadili mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa madeni ya Serikali ili kuongeza uwezo wa taasisi kujiendesha kwa ufanisi na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa za afya nchini.
3. Ujenzi wa Maghala ya Kisasa
Kutokana na ongezeko la mahitaji ya uhifadhi wa bidhaa za afya, MSD itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kisasa yatakayoongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa kwa viwango vinavyokidhi ubora na usalama wa bidhaa hizo.
4. Uwekezaji Katika Nishati Mbadala
Baraza limepongeza hatua za MSD kuja na mkakati wa kuwekeza katika nishati mbadala kupitia Victory Project, ambapo taasisi hiyo itanunua magari yanayotumia gesi pamoja na matumizi ya teknolojia ya sola, hatua zinazolenga kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza uendelevu wa shughuli za taasisi.
Hatua hiyo inaendana na juhudi za kitaifa na kimataifa za matumizi ya nishati safi pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji katika taasisi za umma.
5. Mageuzi ya Kitaasisi na Kidigitali
Katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, MSD inaendelea kutekeleza mageuzi ya kitaasisi (Institutional Reform) sambamba na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali kupitia utekelezaji wa mfumo mpya wa ERP utakaosaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za taasisi.
6. Kuendeleza Uzalishaji wa Bidhaa za Afya
Baraza pia limejadili umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa za afya kupitia MSD Medipharm ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa hizo nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha usalama wa bidhaa za afya nchini na kujenga uwezo wa ndani wa uzalishaji kufuatia mabadiliko ya mahitaji ya dunia baada ya changamoto za mifumo ya ugavi wa kimataifa zilizojitokeza katika kipindi cha UVIKO-19, na vita za Irani na marekani.
Baraza la Wafanyakazi la MSD limeendelea kutajwa kuwa jukwaa muhimu la kujenga ushirikiano kati ya uongozi na watumishi kwa kujadili ustawi wa watumishi, mazingira ya kazi na mikakati ya maendeleo ya taasisi.
Kupitia kikao hicho, MSD imeonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza ufanisi wa taasisi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kupitia upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa wakati.