Ruka kwenda maudhui makuu

MSD Yazindua Mafunzo ya Kitaifa Kuimarisha Usalama na Weledi wa Madereva Wake

Bohari ya Dawa (MSD) imeendesha mafunzo ya siku mbili kwa madereva wake wote wa Makao Makuu na Kanda zake kumi, yakilenga kuongeza weledi, usalama barabarani na ubora wa huduma wanazotoa. 

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa, Mavere Tukai, alisema madereva ni sehemu muhimu ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuhakikisha bidhaa za afya zinawafikia wananchi kwa wakati. 

"Ninyi ni mabalozi wa Bohari ya Dawa (MSD), mnapokuwa barabarani. Kila safari mnayoifanya inabeba dhamana ya kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kwa wakati. Ni wajibu wenu kuendesha kwa usalama, kulinda mali za taasisi na kuendelea kujifunza ili kuongeza ufanisi wa kazi zenu," alisema Tukali. 

Katika mafunzo hayo, washiriki walipata elimu kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu kutoka taasisi tofauti, zikiwemo sheria na usalama barabarani, matumizi bora ya mafuta, matumizi sahihi ya magari ya Toyota Land Cruiser, huduma kwa wateja, maadili ya utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, elimu ya uwekezaji kupitia UTT AMIS pamoja na elimu kuhusu Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF). 

Aidha mafunzo hayo yalihudhuriwa na Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Mtatibu wa Kanda, ambaye pia ni Meneja wa Kanda ya Dodoma, pamoja na viongozi wengine wa Bohari ya Dawa, wakionesha dhamira ya taasisi ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo na uadilifu kwa watumishi wake. 

Akifunga mafunzo hayo, Kamanda wa Kitaifa wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Traffic Police Commander), William Mkonda aliwataka madereva kuyafanyia kazi maarifa waliyoyapata kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, nidhamu na weledi wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

"Maarifa mliyoyapata yatakuwa na maana endapo yataonekana katika matendo yenu. Kuendesha kwa kufuata sheria si kulinda maisha yenu pekee, bali ni kulinda maisha ya watumiaji wengine wa barabara na kuhakikisha mali za taasisi zinatunzwa. Kuwa madereva wanaotanguliza usalama ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa," alisema kiongozi huyo. 

Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Bohari ya Dawa wa kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wake ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, kuimarisha usalama katika shughuli za usafirishaji na kuhakikisha dawa na bidhaa za afya zinawafikia wananchi kwa wakati, ubora na usalama unaostahili. 

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.