Ruka kwenda maudhui makuu

MSD na Uongozi wa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Wajadili Kuimarisha Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya

Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam imefanya kikao maalum na viongozi wa sekta ya afya wa mkoa huo, kwa lengo la kujadiliana kwa kina namna bora ya kuimarisha huduma za upatikanaji wa bidhaa za afya, kuanzia hatua ya uwasilishaji wa maombi ya bidhaa kwa wakati (Timely Order Submission) kutoka vituo vya kutolea huduma za afya, hadi hatua ya uwasilishaji wa mahitaji hayo kwa vituo husika kwa wakati uliopangwa (Timely Delivery).

Kikao hicho muhimu kiliandaliwa kama sehemu ya jitihada za MSD za kuendelea kuboresha ushirikiano na wadau wa sekta ya afya, ili kuhakikisha mfumo wa ugavi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi unakuwa thabiti, wenye ufanisi na unaokidhi mahitaji halisi ya wananchi kwa wakati unaostahili.

Ujumbe wa MSD katika kikao hicho uliongozwa na Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Betia Kaema, akiambatana na wataalamu wa MSD wanaosimamia Mfumo wa Uagizaji wa Bidhaa (Logistics Management System - LMS), ambao una jukumu kubwa la kuratibu mchakato mzima wa maombi na usambazaji wa bidhaa za afya kati ya MSD na vituo vya huduma.

Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, ujumbe uliwakilishwa na viongozi mbalimbali wa kitaalamu wakiwemo Mfamasia wa Mkoa (RPharm), Mtaalam wa Maabara wa Mkoa (RLT), pamoja na Wafamasia wa Wilaya (DPharms) na Wataalamu wa Maabara wa Wilaya (DLTs) kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Kupitia majadiliano ya kina yaliyofanyika katika kikao hicho, pande hizo mbili zilikubaliana kwa pamoja kuimarisha zaidi ushirikiano na mawasiliano baina ya MSD na viongozi wa afya wa ngazi za mkoa na wilaya, pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo chini yao.

Makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha kuwa taarifa za mahitaji ya bidhaa za afya (maoteo) zinaandaliwa kwa usahihi wa hali ya juu, zikizingatia mwenendo halisi wa matumizi katika vituo husika, na kuwasilishwa MSD kwa wakati uliopangwa. Hatua hii itaiwezesha MSD kupanga vyema mipango yake ya ugavi, kuhakikisha bidhaa zinazopatikana zinaendana na mahitaji halisi ya vituo, na hivyo kuepusha changamoto za uhaba wa bidhaa muhimu za afya au usambazaji unaokwenda nje ya kalenda iliyopangwa.

Aidha, ilibainika kuwa uwiano mzuri kati ya uwasilishaji wa maombi kwa wakati na ufanisi wa usambazaji ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi bila vikwazo, hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya dawa na vifaa tiba kama Mkoa wa Dar es Salaam.

Ushirikiano huu unaenda sambamba na dhamira kuu ya MSD ya kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa wananchi, kwa wakati unaofaa na kwa gharama nafuu, kupitia mfumo wa ugavi ulio imara, wenye uwazi na unaozingatia weledi.

MSD imeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu na wadau wote wa sekta ya afya katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na viongozi wa mikoa na wilaya, ili kuhakikisha mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini unakuwa na tija zaidi, unaoweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza, na hatimaye kuchangia katika ujenzi wa mfumo wa afya ulio imara, stahimilivu na endelevu kwa taifa.

Add new comment

Restricted HTML

  • You can align images (data-align="center"), but also videos, blockquotes, and so on.
  • You can caption images (data-caption="Text"), but also videos, blockquotes, and so on.

About

MSD ilianzishwa kwa madhumuni ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya zilizoidhinishwa zinazohitajika kutumiwa na vituo vya afya. Katika kutekeleza dhamira hii, tunahakikisha kuwa bidhaa za afya nchini Tanzania zinapatikana, zinategemewa, na zinauzwa kwa bei nafuu lakini pia zinatolewa kwa wakati katika vituo vyote vya afya nchini Tanzania na kwingineko.

Featured Posts

Contact info

Dhamira yetu: Kufanya bidhaa bora za afya kufikiwa na vituo vyote vya afya vya umma nchini Tanzania.