MSD KUOKOA SHILINGI Bil.2.3, UJENZI WA GHALA JIPYA LA KANDA YA DAR ES SALAAM
Bohari ya Dawa (MSD) inatarajia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa mwaka, ikiwa ni gharama ambazo zimekuwa zikitumika kukodisha maghala binafsi kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa za afya.
Tathimini hiyo imetolewa na uongozi wa MSD baada ya kukabidhi rasmi hati ya mradi wa ujenzi wa ghala jipya la kisasa (site), pamoja na kibali cha ujenzi kwa Kampuni ya Hainan International kutoka China, cha ujenzi wa ghala jipya na la kisasa la Kanda ya Dar es Salaam.
Ujenzi wa ghala hilo la kisasa lenye ukubwa wa mita za mraba 3,900, unatekelezwa katika eneo la Keko, karibu na Makao Makuu ya MSD mkoani Dar es Salaam, na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 12 kutoka sasa.
Akizungumzia ujenzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai alisema mradi huo umezingatia matumizi ya teknolojia za kisasa na nishati mbadala ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati, kupunguza gharama za uendeshaji na kuunga mkono jitihada za uhifadhi wa mazingira.
Aliongeza kwamba fedha zote za utekelezaji wa mradi huo zipo tayari, jambo linalotoa uhakika wa mradi kukamilika kwa wakati.
Kukamilika kwa ghala hilo kutaimarisha uwezo wa MSD wa kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya, kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja na wadau wa sekta ya afya, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wananchi.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja na wadau wa sekta ya afya kwa kuwezesha usimamizi bora wa bidhaa na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika mnyororo wa ugavi.
Ujenzi wa ghala la Kanda ya Dar es Salaam ni sehemu ya mpango mpana wa MSD wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, mageuzi ya kiutendaji na teknolojia ili kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wananchi na kuchangia utekelezaji wa ajenda ya Taifa ya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa Watanzania wote.
Mradi huo pia unadhihirisha dhamira ya MSD ya kujenga taasisi endelevu, yenye ufanisi wa juu wa kiutendaji na inayotumiarasilimali kwa tija katika kutekeleza jukumu lake la msingi la kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wakati, ubora unaotakiwa na kwa gharama nafuu.