MSD Dodoma Yaadhimisha Wiki ya Famasi kwa Kuchangia Damu Salama
Dodoma, Juni 2026
Watumishi wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dodoma, wakiongozwa na wataalamu wa famasi, wameungana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kuadhimisha Wiki ya Famasi inayofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 16 Juni 2026.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na shughuli za kijamii na utoaji wa elimu kwa umma, ikiwa ni pamoja na kampeni ya uchangiaji wa damu salama kwa hiari. Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa damu salama kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu, baadhi ya watumishi wa MSD Kanda ya Dodoma walijitokeza na kuchangia damu kwa hiari.
Ushiriki huo pia umefanyika ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mchangia Damu Duniani, ambayo huwahimiza wananchi kutambua umuhimu wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wanaohitaji huduma za dharura, wajawazito, watoto na wagonjwa wengine wanaohitaji kuongezewa damu.
Wiki ya Famasi huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango mkubwa wa taaluma ya famasi katika kuboresha huduma za afya. Maadhimisho hayo huambatana na shughuli mbalimbali za utoaji elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa, usalama wa dawa, ushauri wa kitaalamu pamoja na nafasi ya wataalamu wa famasi katika kuimarisha mfumo wa huduma za afya nchini.
Kupitia maadhimisho hayo, wataalamu wa famasi wameendelea kutoa hamasa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia dawa kwa usahihi, kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na kutambua mchango wa famasi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa.
Kwa mwaka 2026, Wiki ya Famasi inaadhimishwa chini ya kaulimbiu isemayo:“Famasi: Ufunguo wa Maono ya 2050 katika Sekta ya Afya.”
Kaulimbiu hiyo inaakisi nafasi muhimu ya taaluma ya famasi katika kufanikisha maendeleo ya sekta ya afya nchini kupitia upatikanaji wa dawa bora, salama na zenye ubora unaokidhi mahitaji ya wananchi, sambamba na kuimarisha huduma za afya kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
MSD itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya katika kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya zenye ubora na kuchangia katika kuboresha afya na ustawi wa Watanzania.