MSD Mtwara Yateta na Wadau Wake, Kuimarisha Huduma
Katika kuhitimisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, MSD Kanda ya Mtwara imefanya ziara maalum katika Kituo cha Afya Ufukoni kwa lengo la kukusanya maoni ya wateja na kujadili namna bora ya kuboresha huduma na mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya. Katika ziara hiyo, timu ya MSD Mtwara ilipata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa kituo hicho pamoja na wananchi wanaonufaika na huduma zake, ili kusikiliza changamoto, matarajio na mapendekezo yao kuhusu huduma zinazotolewa na MSD. Ziara iliyolenga kuimarisha ushirikiano baina ya MSD na wateja wake, kwa kuhakikisha bidhaa muhimu za afya zinafika kwa wakati na kwa ubora unaostahili.
Kwa kutambua mchango wa Kituo cha Afya Ufukoni katika kutoa huduma kwa jamii, MSD Kanda ya Mtwara ilitoa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa vya afya na mahitaji ya msingi kwa kina mama wajawazito wanaotarajiwa kujifungua katika kituo hicho. Misaada hiyo inalenga kuboresha mazingira ya utoaji huduma na kusaidia akina mama kupata huduma salama na bora wakati wa kujifungua. Zaidi ya hayo, MSD imekabidhi mashine ya usingizi (anaesthesia machine) pamoja na kifaa cha kufuatilia hali za mgonjwa (patient monitor), vifaa ambavyo vitatumika katika huduma za upasuaji ambazo zinatarajiwa kuanzishwa hivi karibuni katika kituo hicho. Utoaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya dhamira ya MSD ya kuimarisha miundombinu ya afya kwenye vituo vya kutolea huduma kote nchini.
Katika mwendelezo wa maadhimisho hayo, MSD pia ilifanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mtwara, ambaye ni mmoja wa wateja wao wakubwa, ambapo walikutana na uongozi wa hospitali hiyo kujadili masuala mbalimbali yahusuyo upatikanaji wa bidhaa za afya, changamoto zilizopo na fursa za kuimarisha ufanisi wa mnyororo wa ugavi. MSD itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wake kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kupitia upatikanaji wa bidhaa muhimu za afya kwa wakati.